- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Katika kutambua na kuthamini mchango wa walimu katika kuinua kiwango cha taaluma kwa shule za msingi, Manispaa ya Shinyanga imetoa tuzo na vyeti vya pongezi kwa walimu na shule zilizofanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024, katika hafla maalum iliyofanyika leo Aprili 12, 2025 katika ukumbi wa mikutano shule ya sekondari ya wasichana Shinyanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hizi, Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Mwl. Samson Hango, ameipongeza Manispaa ya shinyanga kwa kuandaa tukio hili muhimu, huku akitumia fursa hiyo kuwasihi walimu kuendelee kujituma na kuweka juhudi zaidi katika ufundishaji, ili kusaidia wanafunzi kufikia malengo yao na kutimiza ndoto zao.
“Tuzo hizi ni alama ya kumbukumbu yenye thamani kubwa kwa walimu na shule kwa ujumla, twendeni tukajitume, tukawe wazalendo – elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu,” amesema Mwl. Hango.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Elias Masumbuko amewapongeza walimu kwa manispaa ya shinyanga kwa moyo wa kujitolea kuwafundisha wanafunzi na muda wa kazi hali inayochochea kupanda kwa ufaulu kwa kila mwaka.
Naye Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Shinyanga Mwl. Merry Maka amewapongeza walimu kwa juhudi na moyo wa kujitolea katika kuhakikisha watoto wanapata maarifa ya kusoma, kuandika, na kuhesabu, sambamba na kuwaandaa kuwa viongozi bora wa baadae huku akiwataka walimu kuongeza juhudi zaidi ili kufikia malengo ya ufaulu ya asilimia 95 kwa mwaka wa elimu 2025, ikiwa ni malengo ya idara ya elimu Msingi manispaa ya Shinyanga.
Kwa mujibu wa takwimu Manispaa ya Shinyanga kwa shule za msingi zimeendelea kufanya vizuri kitaaluma: Mwaka 2022: Ufaulu wa jumla ulikuwa 84.68%. Mwaka 2023: Ufaulu wa jumla ulikuwa ni 84.25, huku Ufaulu kwa mwaka 2024 ukipanda hadi 88.42%, ikiiweka Manispaa ya Shinyanga katika nafasi ya kwanza kimkoa kati ya Halmashauri sita za Mkoa wa Shinyanga.
Hafla hii imelenga si tu kutoa pongezi bali pia kuwa chachu ya kuongeza hamasa kwa walimu na shule nyingine kuendelea kufanya vizuri zaidi.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga