- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Kamati ya Fedha na Utawala Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo ndani ya Manispaa hiyo kuipa kipaumbele miradi ya elimu ili ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma bora kwa wanafunzi.
Wito huo umetolewa na Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Pendo John Sawa, leo Januari 21, 2026, wakati wa ziara ya Kamati ya Fedha na Utawala iliyotembelea miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ndani ya Manispaa kwa lengo la kujionea hali ya utekelezaji na maendeleo yake.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Pendo amesema kuwa licha ya miradi yote kuwa na umuhimu mkubwa kwa jamii, miradi ya elimu inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kutokana na uhitaji wake wa haraka, hususan kwa wanafunzi wanaohitaji mazingira bora, salama na rafiki ya kujifunzia.
“Miradi yote ya maendeleo ni muhimu kwa jamii yetu, lakini ni lazima tuweke mkazo zaidi kwenye miradi ya shule ili ikamilike kwa wakati na watoto wetu wapate maeneo bora na salama ya kusomea,” amesema Mhe. Pendo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Ndg. Peres Kamugisha, amesema Menejimenti ya Manispaa itaendelea kushirikiana na Kamati ya Fedha, Waheshimiwa Madiwani pamoja na wadau wengine kwa lengo la kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Amesema hatua hiyo inaendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika mazingira salama na rafiki.
Nao baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wameipongeza Menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa juhudi zake za kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na usimamizi wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Katika ziara hiyo, Kamati ya hii imetembelea jumla ya miradi mitano (05) ikiwemo ujenzi wa Shule Mpya ya Butulwa, ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Bugayambelele, ujenzi wa Nyumba ya Mkurugenzi, ukarabati wa vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Mwamapalala, pamoja na kukagua ujenzi wa Stendi Mpya ya Mabasi ya Mikoa.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga