- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Josephine Matiro ameongoza mkutano wa wadau wa elimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna wa Manispaa. Wadau mbalimbali wa elimu katika Manispaa ya Shinyanga wamejadiliana mambo mbalimbali ya kuinua kiwango cha elimu kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na chuo cha veta. Kwa pamoja waliazimia mambo mbalimbali ikiwemo kuwa kwa kila mzazi anapaswa kutii wito wa kuitwa shuleni kwa lengo la kutoa ushirikiano kwa walimu. Kwa jambo lolote ikiwemo masuala ya nidhamu za wanafunzi na mikutano mbalimbali ambayo uongozi wa shule utaona unafaa kuwaita wazazi, ni lazima wazazi waitikie wito huo bila kukosa. Mkutano uliazimia kuwa kwa mzazi asiyetii wito wowote kutoka katika shule ambayo watoto wao wanasoma, taarifa zitolewe mara moja katika vituo vya dola na mzazi huyo akamatwe.
Pamoja na agizo la kukamatwa kwa mzazi ayesitii wito wa shule, pia mkutano uliazimia kuanzia vituo vya elimu ya watu wazima ambayo itawasaidia wazazi na walezi kujifunza stadi za maisha kwa kushirikiana na chuo cha ufundi stadi cha VETA Shinyanga. Majadiliano yaliendelea pia katika eneo la upimaji wa walimu kwa kuwapa malengo ya ufaulu wa wanafunzi na kwa kila mkuu wa shule ambaye atashindwa kupanga na kusimamia utekelezaji wa malengo, atalazimika kuondolewa madaraka ya kuongoza katika shule hiyo.
Changamoto ya wanafunzi wa kike kupata ujauzito ni mada ambayo wadau wa elimu walichangia kwa muda mrefu na kuamua kuwa ipo haja ya mwanafunzi wa kike aliyepata ujauzito kuchukuliwa hatua za kisheria kama mtuhumiwa wa kuficha ushahidi iwapo atabainika kupotosha taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa mhusika alimpa mimba. Mkuu wa Wilaya alitoa ufafanuzi kuwa mahakama inapata wakati mgumu sana wa kutoa maamuzi kutokana na jamii ya wanashinyanga kuwa na tatizo la kutokukubali kutoa ushahidi mahakami pindi wanapotakiwa kufanya hivyo. "Haupo ushirikiano wa wazazi na binti mwenyewe aliyepewa ujauzito wakati wakitakiwa kutoa ushahidi mahakamani. Hali hii inachangia mashauri mengi kuchukua muda mrefu kutolewa hukumu ingawa suala hili lingeweza kupata ufumbuzi wa wahusika kupewa hukumu stahiki kama wazazi wa binti na binti mwenyewe wangetoa ushirikiano. Mahakama inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi. Upo mshikamano kwa wanajamii kulindana na kukataa kutoa ushahidi. Jamii ya namna hii inatakiwa kubadilika kwa ajili ya ukombozi wa watoto wetu wa kike". alieleza Mkuu wa Wilaya.
Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa akijibu hoja mbalimbali za wadau wa elimu.
Naye Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa Mwalimu Victor Emmanuel alitoa ufafanuzi wa majukumu ya jamii kuwa ndio wamiliki wa shule zilizopo katika maeneo yao kwa kuwaambia kuwa suala la ulinzi wa mali za shule ni jukumu la wanajamii na si vinginevyo. Pamoja na ulinzi wa shule, pia jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanapewa chakula cha mchana ni vema jamii kupitia kamati za shule kuomba kibali katika mamlaka, kibali ambacho kitawataka wazazi wachangie chakula cha watoto mashuleni."Shule ni ya jamii. Suala la ulinzi wa shule ni jukumu la jamii inayomiliki shule" Alisema Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa.
Afisa Elimu Msingi Mwalimu Yesse Kanyuma akiwasilisha mada mbele ya mkutano wa wadau wa elimu
Afisa Elimu Msingi wa Manispaa Mwalimu Yesse Kanyuma alisema kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika suala la ufundishaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) ili kuhakikisha kuwa asiwepo mwanafunzi hata mmoja asiyejua kusoma, kuandika na kuhesabu afikapo darasa la tatu. Hii ina maana kuwa kwa kila mwanafunzi atakayehitimu elimu ya msingi asiwepo asiyekuwa na stadi za KKK. "Mkuu wa shule atakayeruhusu kuingia darasa la tatu mwanafunzi asiyejua kusoma, kuandika au kuhesabu, mwalimu mkuu huyo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kushtakiwa mahakamani". Alisema Afisa Elimu Msingi wa Manispaa.
Sambamba na mkutano huo pia zawadi kwa washindi zilitolewa na Mkuu wa Wilaya alikuwa mgeni rasmi kuwatunuku washindi vyeti vya kufanya vizuri. Zawadi hizo zilitolewa kwa kuzingatia ufaulu wa shule na ufaulu wa wanafunzi. Kwa shule za sekondari, shule tatu bora za serikali na shule binafsi bora zilipewa vyeti vya ushindi kwa kufanya vizuri katika mitihani ya taifa iliyofanyika mwaka 2016. Shule za seikali ni shule ya sekondari Uhuru (3/22 kiwilaya, 12/103 kimkoa na 411/3280 kitaifa), masekelo 7/22 kiwilaya,25/103 kimkoa na 948/3280 kitaifa) na Chamaguha (8/22 kiwilaya,44/103 kimkoa na 1329/3280 kitaifa). Nazo shule binafsi zilizopata zawadi ya vyeti vya kufanya vizuri ni shule ya sekondari KOM (1/22 kiwilaya, 2/103 kimkoa na 83/3280 kitaifa), St. Francis of Asis (2/22 kiwilaya, 11/103 kimkoa na 353/3280 kitaifa) na Buluba (4/22 kiwilaya, 17/103 kimkoa na 513/3280 kitaifa). Pia wanafunzi watatu bora katika shule za sekondari za serikali na watatu bora katika shule za sekondari binafsi walizawadiwa vyeti vya kufanya vema.
Mwalimu Jasson Rwegasira akipokea zawadi ya cheti cha shule ya Uhuru kwa kuwa mshindi wa kwanza kiwilaya katika kundi la shule za sekondari za serikali.
Pia kwa upande wa shule za msingi, Jumla ya shule za msingi 15 zilipewa zawadi kwa mchanganuo wa shule 3 za serikali zilizofanya vizuri, shule 2 zisizo za serikali zilizofanya vizuri na shule 10 ambazo zimeonyesha maendeleo mazuri ya ufaulu wa wanafunzi katika mitihani iliyofanyika mwaka 2016 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2015. Kwa kutambua mchango wao wa kupanda juu katika viwango vya ufaulu wa wanafunzi, shule hizo 10 zilipewa vyeti ikiwa ni kuthamini juhudi walizozifanya ili waendelee kujitahidi zaidi kwa mwaka wa masomo wa 2017.
Mheshimiwa Mwendapole-Diwani wa kata ya Kambarage akichangia mada katika mkutano
Wadau mbalimbali wa Elimu wa Manispaa wakisikiliza mada zilizowasilishwa katika mkutano
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga