- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kasi huku wakizingatia viwango bora vya huduma wanazozitoa.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, ndugu Jomaary Mrisho Satura katika kikao kazi kilichofanyika katika viwanja vya Ofisi Kuu ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Kikao hicho kilichojumuisha Wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Shule, Walimu wakuu, Maafisa Elimu Kata, Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji, Waganga wafawidhi, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Afya, Kilimo na mifugo ngazi ya kata, CHMT na watumishi wa makao makuu ya Halmashauri hiyo.
"Mimi napenda sana kasi ya utoaji huduma lakini yenye viwango vya juu sana. Kwahiyo niwasihi sana kila mmoja katika nafasi yake ahakikishe anafanya kazi kwa juhudi, maarifa na weledi mkubwa katika kutoa huduma kwa wananchi." Alisema Satura.
Satura aliwataka watumishi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kushirikiana na kushikamana pamoja kufanya kazi ili kuifanya halmashauri hiyo kuwa ya mfano. Aliongeza kuwa ubora wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga utapimwa kwa matokeo ya utoaji huduma kwa wananchi.
"Matokeo ya utoaji huduma kwa wananchi ndiyo yatakayotufanya tuonekane bora au dhaifu. Kwa mfano, watakao tufanya kuwa wa kwanza katika elimu ni walimu. Watakaotufanya kuwa wa kwanza katika usafi wa mazingira ni watu wa afya. Kwa hiyo utaona kuwa ili tufikie malengo ya kuwa Halmashauri ya mfano ni lazima kila mtumishi katika sehemu yake atekekeleze wajibu wake ipasavyo." Alisema Satura.
Satura alitoa wito kwa watumishi wote wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa wanakuwa na mtazamo chanya kwa kutambua wajibu wao huku wakitekeleza majukumu yao kwa nidhamu ya hali ya juu kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.
"Kila mtu awe na positive altitude (mtazamo chanya), binafsi huwa nawatambua haraka na kuwaheshimu watu wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa ubunifu mkubwa. Na huwa sina urafiki na watu wasiotekeleza wajibu na majukumu yao, watu wazembe wanao acha kutekeleza majukumu yao kwa makusudi. Kwa mfano, sina urafiki na watumishi wanaotumia vibaya muda wa kazi kwa kufanya mambo ambayo hayapo katika utumishi wa umma badala ya kutumia muda huo kufanya kazi na kutoa huduma kwa wananchi". Aliongeza Satura.
Kuhusu stahiki na maslahi ya watumishi Satura alisema kuwa atajitahidi kuhakikisha kuwa stahiki zote za watumishi kama vile madeni yatokanayo na mapunjo ya mishahara, likizo na upandishwaji madaraja (vyeo) zinashughulikiwa kwa wakati kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo na kwa mujibu wa maelekezo ya serikali na uwezo wa kifedha wa Halmashauri hiyo.
Aidha Satura aliongeza kuwa anatarajia kufanya ziara ya kutembelea watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga katika maeneo yao ya kazi kama vile mashuleni, vituo vya afya, ofisi za kata ili aweze kusikiliza na kupokea kero za watumishi hao kisha kuzifanyia kazi. Alisema wataanda utaratibu wa kuanzisha bango kitita kwa ajili ya kupokea kero, changamoto na malalamiko mbalimbali ya watumishi.
Wakati huo huo Satura alitumia kikao hicho kueleza muelekeo wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga huku akizitaja sekta za Elimu, Afya na Uchumi kuwa za kwanza katika vipaumbele vya Halmashauri hiyo.
Alisema kuwa majukumu ya kwanza ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga yatakuwa ni kuhakikisha kuwa huduma za afya na usafi wa mazingira zinaboreshwa na kusimamiwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na kupeleka huduma za afya katika maeneo ambayo hayana huduma hizo kwa kujenga vituo vya afya na zahanati.
Kwa upande wa elimu alisema kuwa Halmashauri itahakikisha inaboresha na kusimamia utolewaji wa elimu kwa kuhakikisha kuwa shule zote za Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga zinakuwa miongoni mwa shule bora nchini.
Kuhusu uchumi na ukusanyaji wa mapato, Satura alisema kuwa hatakuwa na uvumilivu kwa mtu yeyote atakaye hujumu ukusanyaji mapato. Alitoa wito kwa watumishi wote kutoa taarifa haraka iwezekanavyo katika ofisi yake mara tu wanapo baini hujuma katika ukusanyaji mapato.
"Bila kusimamia ukusanyaji wa mapato hatuwezi kutoa huduma tunazozitaka kwa wananchi kama vile kujenga madarasa, zahanati, barabara na miundombinu yake pamoja na kulipa stahiki zingine za watumishi. Nitoe wito kwa wanaosimamia ukusanyaji wa mapato wahakikishe kuwa wanafanya kazi hii kwa uaminifu na weledi mkubwa." Alisema Satura.
Satura aliwaagiza watumishi wote wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanatunza vizuri mali za umma zote wanazokabidhiwa kuzisimamia na kuzitumia kama vile magari, samani na majengo ili kupunguza gharama za uendeshaji na matengenezo hatua ambayo itaifanya Halmashauri hiyo kutumia vizuri mapato inayoyakusanya kwa kugharamia miradi ya maendeleo na kulipa stahiki za watumishi.
Akitoa neno la shukurani baada ya hotuba ya Mkurugenzi, Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Bi Getruda Gisema aliwataka watumishi wenzake kujifanyia tathmini (self assessment) katika uwajibikaji wao ili waweze kubadilika na kufanya kazi kwa weledi wa kasi kubwa kama ilivyoelekezwa na Mkurugenzi Satura.
Bi Gisema aliwataka watumishi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kufanyia kazi maelekezo (orientation) yaliyotolewa kwani maelekezo kama hayo utolewa kuanzia mtumishi anapoajiriwa hadi anastaafu.
"Wito wangu kwa watumishi wote tuliopo hapa leo ni kuwa tukawe mabalozi wazuri kwa kuwaeleza watumishi wenzetu tuliowaacha katika vituo vyetu vya kazi kwa kuwaeleza mwelekeo na maelekezo mazuri ya mwajiri wetu ili kufikia malengo tarajiwa ya Manispaa yetu". Alisema Bi Gisema
Awali akitoa neno la utangulizi wakati akimkaribisha Mkurugenzi Satura kuongea na watumishi Bi Gisema, alisema kuwa Halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi hususani katika idara ya ujenzi, kitengo cha manunuzi na watendaji wa mitaa na vijiji.
Changamoto zingine ni:- upungufu wa ofisi kwa watumishi, madeni ya watumishi yatokanayo na mishahara na yale yasiyo ya mishahara kama vile uhamisho, matibabu na likizo, uwepo wa wafanyakazi sita wanaolipwa kupitia makusanyo ya ndani na ufinyu wa bajeti wa kuendesha mafunzo kazini.
MATUKIO KATIKA PICHA
Watumishi wakisikiliza kwa makini nasaha za Mkurugenzi
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga