- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na Walimu wakuu katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuhakikisha wanafunzi wote wa Shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri hiyo wanapata chakula Shuleni kwa kuhamasisha wazazi na walezi kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao ili kuwapa utulivu wa kujifunza wawapo shuleni.
Maelekezo hayo yametolewa jana, Agosti 25, 2023 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mwalimu Alexius Revocatus Kagunze wakati anaongea na Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule za Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwenye Mkutano wa kawaida wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Manispaa ya Shinyanga uliofanyika katika Shule ya Sekondari Buluba mjini Shinyanga.
"Upatikanaji wa Chakula Shuleni ni moja ya utekelezaji wa KPI (vigezo vya upimaji) za mikataba yenu mliyojaza kwa ajili ya kusimamia taaluma shuleni. Chakula shuleni ni muhimu sana kwa ajili ya kuleta utulivu kwa mwanafunzi kujifunza anapokuwa darasani. Nawaagiza kuhakikisha mnaitisha vikao vya wazazi kuhamasisha wazazi kuwachangia watoto wao chakula shuleni." Alisisitiza Kagunze.
Kuhusu usafi na utunzaji wa mazingira, Kagunze amewaelekeza Wakuu wa Shule na Walimu wakuu kuhakikisha mazingira ya Shule zao yanakuwa safi muda wote na kukitumia kipindi hiki cha kiangazi kuandaa mashimo ambayo watapanda miti ya kutosha pindi msimu wa mvua utakapoanza.
"Tumieni kipindi hiki cha kiangazi kuandaa mashimo kwa ajili ya kupanda miti mingi msimu wa mvua utakapoanza. Yaandaeni vizuri, mtie mbolea na inasisitizwa kuwa tupande miti ya matunda ya kutosha pamoja na ya kimvuli pia. Aidha, tuendelee kuitunza miti ambayo tumekwisha ipanda ili kutunza mazingira yetu." Aliongeza Kagunze.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Kagunze amewataka viongozi wa elimu hususani Walimu wakuu na Wakuu wa Shule kujenga umoja, upendo na ushirikiano huku wakitenda haki kwa walimu wote wanaowaongoza katika Shule zao.
Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) ulianzishwa mwaka 2005 ukiwa na malengo ya kuwakutanisha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa uongozi mashuleni. Kwa mujibu wa Katiba ya Umoja huo, muundo wake umegawanyika katika ngazi ya Halmashauri, Mkoa, Kanda na Taifa.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga