- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga ni miongoni mwa Halmashauri Nchini iliyoshiriki kikamilifu katika kuadhimisha kilele cha Sherehe za Siku ya Wanawake Duniani ambayo Kimkoa ilifanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Machi 8, 2023.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi 39.
Akizungumza wakati wa Sherehe hizo, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude, aliseama kuwa wanawake ni kundi kubwa lenye nguvu zaidi katika nyanja mbalimbali ikiwamo Uongozi, Uchumi, Kijamii na kadhalika hivyo katika kuadhimisha siku yao ni muhimu sana wakapongezwa na kupewa nguvu zaidi ili wakaongeze jitihada.
Hivyo basi katika kuhakikisha kuwa Serikali inawajali na kuwaongezea nguvu kwa kuwapatia mitungi ya Gesi bure kabisa jambo ambalo litaenda kuboresha na kuongeza tija kwa shughuli zao za kila siku katika kujipatia kipato cha familia zao na Taifa pia, kwani wataondokana na matumizi ya mkaa au kuni jambo ambalo linatumia muda mrefu zaidi katika kupika kulinganisha na matumizi ya Gesi.
“Ukitazama hasa katika kipindi hiki Wanawake wamekuwa na mchango mkubwa sana katika jamii zetu na Nchi kwa ujumla kama ambavyo unamuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kiongozi bora zaidi, kuna Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Akson anaongoza vema kabisa Bunge letu na wengine wengi zaidi Tanzania na nje ya Nchi hii ni kielelezo kuwa wanawake ni kundi kubwa na muhimu zaidi.
"Kwa msingi huu sasa nawapongeza sana Manispaa ya Shinyanga kwa kuamua kuwapatia mitungi ya gesi bure kwa wanawake wajasiriamali wao kutoka katika Kata zao zote 17 za Manispaa, jambo ambalo ni la kuigwa na Halmashauri nyingine kwani watakuwa wanakwenda na Kauli Mbiu isemayo Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia, Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia maana yake Manispaa wamekuwa wabunifu na kuwaletea mabadilko wajasiriamali wao ambayo ni chachu kwao " alisema Mhe. Mkude.
Mhe. Mkude aliwakumbusha pia wananchi wote waliofika katika sherehe hiyo juu ya umuhimu wa kuchukua tahadhari zaidi kwa ugonjwa wa Homa Kali na Joto yaani UVIKO 19 kwani ugonjwa huo upo na kwamba kwa wale ambao hawajamalizia Chanjo ya pili wafanye hivyo haraka kutoka na umuhimu wake.
"Tuendelee kuchukua tahadhari zaidi kwa ugonjwa huu, na ikumbukwe kwamba hakuna madhara yoyote kwenye Chanjo hizo zinazotolewa na Serikali kupitia Sekta ya Afya katika vituo vyote vya Afya na zaidi ya yote huduma hii ni bure kabisa kwa wananchi, hakuna malipo yoyote," alisisitiza Mhe. Mkude.
Kwa upande wake Naibu Mstahiki Meya Mhe. Ester Makune alisema kuwa, Manispaa ya Shinyanga katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani imeamua kutoa Mitungi hiyo 39 ya Gesi kwa wawakilishi wa wanawake wajasiriamali wawili kutoka katika kila Kata, hatua hiyo inafuatia juhudi zao katika ujasiriamali wanaoendelea nao katika kukuza kipato cha familia na Taifa kwa ujumla.
Naibu Mtahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mh. Ester Makune, akizungumza kwenye mkutano.
Katika hatua nyingine hadhara hiyo ilitumia muda huo kufanya Harambee ya Ujenzi wa Bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mwamashele, ambapo Manispaa ya Shinyanga ilichangia kiasi cha Tzs 500,000/= Taslimu ikiwa ni mchango wao.
Siku ya Wanawake Duniani ilianza kuadhimishwa rasmi duniani mwaka 1975 ambapo Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi siku hiyo kuwa ni Siku ya Wanawake Duniani ambapo Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa inasherehekea kama Nchi nyingine Duniani.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga