- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Na George Mganga, Shinyanga Manispaa
NAIBU Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Utaribu). Bw. Kaspar Kaspar Mmuya, amewataka wananchi wa Shinyanga kuhakikisha wanaondoa umimi katika kutekeleza majukumu yao ili kulisaidia Taifa kuzidi kusonga mbele kimaendeleo.
Hayo ameyasema Disemba 9, 2022 katika Maadhimisho ya Uhuru wa miaka 61 Tanzania ambayo yalifanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM) ambapo kulifanya mdahalo huku mgeni rasmi akiwa Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Prof. Siza D. Tumbo.
Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Utaribu). Bw. Kaspar Kaspar Mmuya, akizungumza katika mdahalo wa Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru.
Akizungumza na Watumishi mbalimbali wa serikali, Kamati ya Ulinzi na Usalama, viongozi wastaafu, na wananchi waliojitokeza katika ukumbi huo kwa ajili ya mdahalo uliokumbushia zaidi historia ya taifa na maoni mbalimbali kuhusu maendeleo ya nchi, Mmuya ametoa rai akieleza italisaidia taifa kufika mbali kimaendeleo kuliko kuwekeza nguvu za ubinafsi.
“Naombeni nafasi zetu tulizonazo tuzitumie zaidi katika kuleta maendeleo ya taifa, tuache kuwa na umimi ambao hauwezi kutupeleka popote kimaendeleo.
“Tumekuwa na umimi zaidi, tumeacha kulifikiria taifa letu na badala yake tunajifikiria zaidi wenyewe kitu ambacho hakitaweza kustawisha maendeleo yetu. Tulenge mbele zaidi”, alisema.
Katika hatua nyingine Mmuya amewaomba watanzania kuwalea watoto katika malezi yaliyo bora akieleza kuwa kwa sasa kumekuwa na changamoto katika eneo hilo.
Mmuya ameeleza kizazi cha sasa kimekuwa na malezi ambayo yamekuwa ni changamoto kwa kizazi kijacho na akibainisha ili kuepukana na hayo ni vizuri kuwalea katika mazingira ambayo wazee walipitia.
“Tuliangalie eneo la malezi, kumekuwa na changamoto kubwa ambayo inabidi ifanyiwe kazi. Tuwalee watoto wetu katika mazingira ambayo yatawasaidia kuja kuwa na mchango mzuri katika taifa letu”, alisema.
Mbali na malezi, Mmuya amewashauri pia vijana kuacha kulalamika kuwa hakuna kazi na badala yake watumie fursa mbalimbali zilizopo kuzifanyia kazi ikiwemo fursa za kilimo na ufugaji kwa kuwa zinachangia zaidi katika kustawisha maendeleo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mh. Elias Masumbuko alitumia nafasi ya mdahalo huo kupitia historia iliyotolewa na wazee ambao ni wastaafu kukumbuka nchi ilipotoka.
“Tuangalie tulipotoka, utamaduni tunaoishi nao siyo mbaya. Tutambue kuwa hapa tulipofika ni kutokana na jitihada za wazee wetu nasi wananchi kwa ujumla kwa kushirikiana na serikali.
“Nchi hujengwa kwa hekima pia busara, tulinde tunu za taifa na tusherehekee madhimisho ya uhuru wa taifa letu kwa amani”, alisema Mh. Masumbuko.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mh. Elias Masumbuko akizungumza katika mdahalo.
Katika maadhimisho hayo ya miaka 61 ya Uhuru, Katibu Tawala aligawa vyeti vya pongezi kwa Shule za Sekondari za Ngokolo na Uhuru zilizoshiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu na wa pete kama sehemu ya kutambua maendeleo ya taifa lilipotoka na lilipo kwa sasa.
Watu mbalimbali ikiwemo Kamati ya Usalama waliojitokeza kwenye mdahalo wa maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru.
Vilevile, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeadhimisha miaka 61 ya Uhuru kwa kushiriki shughuli za kupata miti katika kambi ya wazee Kolandoto pamoja na kufanya usafi pia kushiriki kwenye tamasha la michezo lililokutanisha shule za Ngokolo na Uhuru.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga