- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Maelfu ya wakazi wa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake, wake kwa waume, leo hii wameshiriki katika mazishi ya aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Marehemu David Mathew Nkulila aliyefariki alfajiri ya tarehe 23/08/2021.
Ilikuwa ni vilio, simanzi na huzuni kutoka kwa waombelezaji muda wote wakati shughuli za mazishi zilipokuwa zikiendelea kuanzia nyumbani kwa marehemu, kanisani hadi makaburini.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali ya Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Philemon Sengati, alisema wana Shinyanga wamepoteza kiongozi mshauri mwenye maono, mpenda haki na usawa.
"Tumepoteza kiongozi, kaka, mshauri mwenye maono na mipango mizuri. Nimefahamina na marehemu Nkulila kwa kipindi kifupi, hakika alikuwa amebahatika kuwa na upendo, mpenda haki na usawa. Alikuwa ni kiongozi aliyependa umoja na mshikamano. Nkulila alipenda kufanya kazi kwa bidii, hakika uongozi wake ulikuwa ni wenye kuacha alama." Alisema RC Sengati.
RC Sengati aliongeza kuwa Serikali ya Mkoa itahakikisha ina muenzi Nkulila kwa kusimamia na kuendeleza mazuri yote aliyoyaanzisha na kuyafanya.
"Nkulila alikuwa anataka kuiona Shinyanga Manispaa inakuwa bora. Alitaka kuiona Shinyanga Manispaa inakuwa jiji. Sisi kama viongozi wa Mkoa tutaenzi maono yake." Aliongeza RC Sengati.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Waziri Mkuu, na Waziri wa TAMISEMI, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana ambaye pia ni mbunge wa Shinyanga Mjini, Mheshimiwa Patrobas Katambi alisema yeye na madiwani wenzake wana deni kubwa la kuhakikisha wanatekeleza mipango yote iliyo achwa na Nkulila kwa ajili ya maendeleo ya wana Shinyanga.
"Tuna deni kubwa sana mimi na madiwani wenzangu la kuhakikisha tunatekeleza mipango mizuri yote tuliyopanga naye marehemu Nkulila katika kutekeleza ilani ya CCM." Alisema Katambi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, ndugu Magesa, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga alisema kuwa chama kimempoteza mwanachama wake aliyekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha chama kinafikia malengo yake ya kuwahudumia wananchi kama ilivyo ainishwa katika ilani ya chama hicho.
"Tumepoteza kiongozi mchapa kazi, mwajibikaji aliyepambwa na sifa ya kusema ukweli. Alikuwa mpenda haki na ulikuwa uumtoi katika haki kama aliiona haki hiyo ipo." Alisema Magesa.
Naye mbunge wa viti maalumu mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Dr. Christina Mnzava alisema wana Shinyanga wanamshukuru Mungu kwa zawadi aliyowapatia ya kuishi na David Mathew Nkulila. Aliiomba familia ya Nkulila kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mtu waliyempenda na nguzo kuu ya familia.
Viongozi wengine waliotoa salamu za rambirambi ni Mwenyekiti wa kamati ya amani mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga na Mwenyekiti wa ALAT ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
Viongozi wote hao walimuelezea marehemu Nkulila kuwa alikuwa kiongozi mpenda haki, mchapakazi, mwajibikaji na atakumbukwa daima kwa utendaji kazi wake.
Akitoa mahubiri katika misa ya kumuombea marehemu Nkulila iliyofanyika katika kanisa la Mama Mwenye Huruma, Parokia ya Ngokolo, Baba Paroko, Padri Adolph Makadango aliwataka viongozi wa kisiasa kuiga tabia ya marehemu Nkulila ya kuwafikia wananchi kusikiliza kero, shida, matatizo na changamoto zinazowakabili badala ya kubakia majukwaani na maofisini.
Aidha, Padri Makadangu, alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wanasiasa wote kuishi maisha ya kupendana wakati wote wa shida na raha.
Aidha, wananchi waliohudhuria mazishi hayo walieleza kuwa marehemu Nkulila alikuwa mtu wa watu, aliyependa kuzungumza na kila mtu bila kujali itikadi za kisiasa, rangi, dini wala cheo.
"Nkulila alikuwa rafiki wa kila mtu, mdogo kwa mkubwa, asiyejikweza kwa madaraka aliyokuwa nayo.Ni ndani ya kipindi kifupi kisichozidi hata mwaka tayari tulikuwa tumekwisha ona matunda yake akiwa kama meya wetu wa Manispaa ya Shinyanga. Itatuchukua muda kumpata kiongozi wa aina yake." Alisema Nkuba Masanja mkazi wa mtaa wa Mabambasi, Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga.
Nkulila,Umevipiga vita vilivyo vizuri,Mwendo Umeumaliza, Imani umeilinda.
RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA, NA MWANGA WA MILELE UMUANGAZIE, APUMZIKE KWA AMANI............AMINA
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga