- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko leo Jumapili Agosti 1,2021 amefunga Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga yaliyoanza Julai 23,2021 katika uwanja wa Zainab Telack kijiji cha Butulwa kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga yakiongozwa na kauli mbiu “Uwekezaji wa Madini na Viwanda Shinyanga kwa Uchumi Endelevu”.
Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho hayo, Biteko amewataka Wawekezaji walioshikilia leseni za uchimbaji madini kuendeleza maeneo hayo badala ya kuwazuia wananchi wenye uwezo wa kuchimba ili kuendeleza maeneo hayo na kwamba Serikali imewapa siku 60 baada ya hapo itafuta leseni hizo.
Amesema kumekuwapo na tatizo kwa baadhi ya wawekezaji wa madini kuhodhi leseni kwa muda mrefu na kutozitumia na pale yanapovumbuliwa madini na wachimbaji wadogo ndipo hujitokeza na kudai eneo hilo ni lao.
Kufuatia hali hiyo, Biteko amesema wametoa siku 60 za kutaifisha leseni za uchimbaji wa madini zilizohodhiwa na wawekezaji kwa muda mrefu bila kuzitumia akibainisha kuwa Serikali imedhamiria kuinua Sekta ya Madini, pamoja na kumaliza migogoro yote ambayo hujitokeza baina ya wachimbaji wadogo na wakubwa.
"Naomba mfikishe salamu kwa wawekezaji wa madini ambao wana leseni za uchimbaji na hawazitumii, tumetoa siku 60 tu zianze kutumika, zaidi ya hapo tunazitaifisha na kutoza gharama ambazo Serikali imeingia kutokana kutolipiwa kodi kwa muda mrefu na kusababisha Serikali kukosa mapato na fedha hizi lazima zilipwe hatutakuwa na msalia mtume, hatutaki migogoro ya uchimbaji madini," amesema Biteko.
Biteko pia amewataka wachimbaji wenye Leseni walipe kodi na waepuke vitendo vya utoroshaji madini akibainisha kuwa atakayetorosha madini atakuwa anachoma madini kwa tochi hivyo akikamatwa hatabaki salama.
"Tumefungua masoko, leo Tanzania tuna masoko ya madini 39, tuna Vituo vya kuuza madini 50, na hata Shinyanga masoko yapo mengi, Mwaka 2019 tulifungua soko la kwanza la madini na hili limetuletea faida kubwa, tuone fahali kulipa kodi, tuone fahali kupeleka madini kwenye masoko yetu, kama Wizara ya Madini tutaendelea kuwahudumia watanzania wanaohitaji kuchimba,’’ ameongeza Biteko.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini mkoa wa Shinyanga 'Shinyanga Region Miners Association – SHIREMA', Hamza Tandiko amezishukuru Taasisi za Kifedha kwa kuanza kuwapatia mikopo Wachimbaji wa Madini huku akiomba serikali kupeleka Umeme wenye nguvu ya kuendesha mitambo kwenye maeneo ya machimbo kwani umeme uliopo sasa ni kwa ajili ya mwanga tu.
Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Said Pamui ambao ni miongoni mwa Wadhamini wakuu wa Maonesho hayo, amesema taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya CRDB zimeanza kuwezesha mikopo vikundi vya Wachimbaji wa Madini na Wajasirimali hivyo kuwakaribisha kupata huduma katika Benki yao ambayo pia inatoa Bima za aina mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati amesema maonesho hayo yamesaidia kuutangaza Mkoa huo na kuonyesha fursa za biashara hasa katika sekta ya madini.
Amesema wataendelea kuboresha maonesho na kuwaunganisha wafanyabiashara na wajasirimali akiongeza kuwa Maonesho hayo ni muhimu kwa sababu mkoa wa Shinyanga una madini mengi na una madini ya pekee ya Almasi ambayo yanaendelea kuchochea ukuaji wa uchumi taifa.
"Kupitia maonesho haya washiriki wamepata fursa ya kutambulisha biashara zao, kuuza bidhaa na kujifunza teknolojia ya kisasa na kujua wapi wapate mitaji",amesema.
Hata hivyo amesema atakuwa mkali kwa watu wanaotorosha madini na atakayekamatwa atafirisika hivyo kuwataka wachimbaji madini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Tazama picha hapa chini
Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko akizungumza wakati akifunga Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga yaliyoanza Julai 23,2021 katika uwanja wa Zainab Telack kijiji cha Butulwa kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga leo Jumapili Agosti 1,2021.
Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko akizungumza wakati akifunga Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga yaliyoanza Julai 23,2021 katika uwanja wa Zainab Telack kijiji cha Butulwa kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga leo Jumapili Agosti 1,2021.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga