- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa hatua mbalimbali inazofanya katika kutekeleza usimamizi wa kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwa kununua magari mawili yanayobeba wanafunzi kuwapeleka shuleni na kuwarudisha karibu na makazi yao.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akisalimiana na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Town iliyo katika Manispaa ya Shinyanga kabla ya kupanda kujionea namna Basi la Wanafunzi linavyosafirisha wanafunzi Mjini Shinyanga.
Waziri Dkt. Gwajima ametoa pongezi hizo leo Jumatatu Disemba 5,2022 wakati akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Town baada ya kupanda gari moja na wanafunzi hao kutoka majumbani mwao kuelekea katika shule hiyo iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga.
"Nawapongeza sana Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa ubunifu huu wa usafiri kwa gharama nafuu shilingi 200 kutoka nyumbani hadi shuleni, nina imani wanafunzi sasa watatumia muda mfupi kwenda shuleni na kuwaepusha na vishawishi mbalimbali wawapo njiani, lakini nimeshuhudia gari hili likiwa na Msimamizi wa wanafunzi ambaye ni Afisa Maendeleo ya jamii, hii ni hatua nzuri sana, ni vyema Halmashauri zingine zikaiga mfano wa Manispaa ya Shinyanga namna ya kusaidia wanafunzi, zisisubiri matamko”, amesema Dkt. Gwajima.
Katika hatua nyingine Dkt Gwajima amezitaka Halmashauri na Mikoa yote nchini kuandaa mifumo ya upatikanaji wa haraka wa taarifa za kulinda watoto utaosaidia kufahamu taarifa za watoto.
“Endapo tutakuwa na mfumo wa kulinda watoto itatusaidia pia kudhibiti utoro shuleni, tutaweza kutambua kama mtoto yupo shule au la! Wazazi pia watasaidia kujua mtoto yuko wapi. Mfumo wa pamoja wa taarifa utasaidia kupata sulushisho la matukio ya ukatili katika jamii", amesema.
Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Town Mjini Shinyanga.
Katika hatua nyingine amewataka wadau kuendelea kupaza sauti juu ya vitendo vya jinsia moja huku akibainisha kuwa hatakubali kuona vitendo vya ushoga na vitendo vingine vya ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya usafiri vinavyobeba wanafunzi lakini pia shuleni.
“Ni marufuku vitendo vya ushoga popote, Nawatangazia waovu wote wanaofaundisha madarasa ya ushoga waache mara moja, hata huyo mwanaume aliyekamatwa huko Geita akifundisha watoto ushoga akiwa amevaa nguo za kike ‘sidiria’ na vitu vya kike kike ni lazima achunguzwe,tutalifuatilia hili jambo haiwezekani watoto wetu waharibiwe kwa kufundishwa mambo yasiyofaa, Hili la ushoga nitalifia. Tutawalinda watoto, na hayo madarasa ya ushoga yafe huko huko", amesema Dkt. Gwajima.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo amesema mkoa wa Shinyanga umejipanga kukutana na wadau mbalimbali ili kutengeneza mfumo wa kutoa taarifa kwa ajili ya kuwalinda watoto.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manipaa ya Shinyanga, John Tesha ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, amesema halmashauri hiyo inaendelea kutoa elimu ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto mara kwa mara katika ngazi ya jamii, kwenye nyumba za ibada na Shule za msingi , Sekondari na vyuo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manipaa ya Shinyanga, John Tesha ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga akizungumza katika shule ya Sekondari Town Mjini Shinyanga.
“Pia halmashauri imetumia nafasi ya utoaji mikopo kwa asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama njia nyingine za kuzuia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto”, amesema Tesha.
“Mfano mwingine wa namna mikopo ya asilimia 10 ilivyosaidia kwenye kuzuia na kutokomeza ukatili kwa watoto ni ule ambao mwezi Aprili 2022, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi Milioni 120 kwa vikundi viwili vya vijana. Vikundi hivyo tulivisimamia na kununua magari mawili (Moja ni Basi aina ya Tata na lingine ni Basi dogo aina ya Nissan – Civilian) yanayofanya kazi ya kubeba wanafunzi”,ameongeza Tesha.
Ameeleza kuwa Vikundi hivyo vya vijana vilipewa maelekezo na kusainiana mkataba na Halmashauri kuhakikisha nyakati za asubuhi kuanzia saa 12 hadi saa 2 asubuhi magari hayo yanabeba wanafunzi kuwapeleka shuleni na nyakati za jioni kuanzia saa 10 na nusu hadi saa 12 jioni magari hayo yanabeba wanafunzi kuwarudisha karibu na makazi yao kwa bei elekezi ya shilingi 200/= / 300/=.
“Lengo la kufanya hivi ni kuwahakikishia wanafunzi usalama wao wanapoenda shuleni na wakati wa kurudi nyumbani na kuhakikisha wanafunzi wanafika shuleni kwa wakati na siku zote za masomo hivyo kuwahakikishia ufaulu mzuri katika mitihani yao”, amesema Tesha.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Town Mjini Shinyanga wakisikiliza nasaha mbalimbali kutoka kwa Waziri Gwajima.
Amesema upatikanaji na utumiaji wa magari hayo ya mkopo kwa vijana yamewapunguzia wazazi gharama za kuwasafirisha watoto kwenda na kurudi shuleni ambapo gharama za kumsafirisha mtoto kwenda na kurudi shuleni kwa siku ni kati ya shilingi 500 - 600/= na kwa mwezi ni kati ya shilingi 10,000 - 12,000/=
“Hii ni gharama nafuu ukilinganisha na gharama walizokuwa wanatumia wengi wao za kutumia baiskeli ambapo huwa ni shilingi 500/= hadi 1000/= kwa safari moja ambapo kwa siku ni shilingi 1000/= -hadi 2000/= na kwa mwezi ni shilingi 20,000/= hadi 40,000/=”, ameeleza.
“Kwa kutumia mikopo ya asilimia 10 pia Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imetoa Bajaji kwa watu wenye ulemavu kwa ajili ya biashara ya usafirishaji wa abiria ambapo pia waliokopa tumewaelekeza kubeba wanafunzi popote wanapowakuta kwa bei elekezi. Pia katika mwaka huu wa fedha 2022-2023 unaoendelea tumejipanga kutoa mikopo ambayo itawezesha kununua magari/ Hiace Sita ambazo zitawajibika kufanya biashara ya abiria ndani ya Manispaa na kuhakikisha zibabeba wanafunzi kwa bei elekezi”, amefafanua Tesha.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akisalimiana na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga