- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
WATENDAJI WA MITAA NA KATA MANISPAA YA SHINYANGA WAJENGEWA UWEZO KUHUSU MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI.
Na. Shinyanga MC
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeendesha mafunzo maalum ya Mfumo wa Anwani za Makazi kwa watendaji wapya na waliopo wa mitaa, vitongoji na kata, ikiwa ni hatua muhimu ya kuwawezesha kutekeleza kikamilifu zoezi la usajili wa anwani katika maeneo yao.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Julai 15, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Lewis Kalinjuna uliopo Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, yakilenga kuongeza uelewa, umahiri na weledi wa watendaji hao kuhusu matumizi sahihi ya mfumo huo wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Alexis Kagunze, amesisitiza kuwa mfumo wa anwani za makazi ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya miji, kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuimarisha usalama na kuwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.
“Kupitia mfumo huu, Serikali inaweza kufuatilia maendeleo ya maeneo mbalimbali, kupanga miundombinu kwa tija, na kuhakikisha huduma kama posta, afya, elimu na uokoaji zinawafikia wananchi kwa haraka na kwa usahihi. Huu ni msingi wa ustaarabu wa miji na maendeleo endelevu,” amesema Mwl. Kagunze.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Ndg. Charles Semzaba, amewahimiza watendaji hao kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha taarifa za anwani zinakusanywa, kuhakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo wa kidijitali kwa usahihi.
Mfumo wa Anwani za Makazi ni mojawapo ya mfumo unaolenga kuiweka nchi kwenye ramani ya kidijitali, kukuza uchumi wa kidijitali, na kuharakisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi kwa njia za kisasa na bora zaidi.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga