- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waganga Wakuu wa Mikoa yote wameagizwa kuhakikisha kila Hopitali inakuwa na dawa maalumu kwa ajili ya wazee pamoja na kuwabaini wazee wote katika mikoa yao ili wapate huduma za afya bila malipo. Naibu Waziri wa Afya Dkt. Hamis Kigwangala ametoa agizo hilo alipotembelea kituo cha Wazee cha Kolandoto kilichopo katika Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga. "Hakuna maana yoyote kama mzee anapimwa na tatizo lake linafahamika halafu akifika kwenye dirisha la dawa anaambiwa dawa zimeisha hapa nenda kanunue" amesema Dkt.Kigwangala.
Dkt. Kigwangala amewahakikishia Wazee kuwa, Serikali itahakikisha kuwa hali ya upatikanaji wa huduma za jamii kama vile chakula, malazi na dawa inaimarika ikiwemo mikakati madhubuti ya kuwapatia huduma bila malipo na kuwalinda. Amesema kulingana na sensa ya mwaka 2013 idadi ya Wazee nchini ni milioni 2.5 ambayo ni sawa na asilimia 5.6 ya wananchi wote na inakadiriwa kuongezeka na kufikia wazee milioni 2.7 mwezi Desemba, 2017, hivyo Wizara ya Afya inasimamia maslahi na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.
Awali, Mwenyekiti wa kituo cha Wazee Kolandoto Mzee Somola Maganga na Katibu wa Wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Sengerema wameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa jitihada kubwa ya kuwajali wazee na kutekeleza yale waliyoomba. Aidha, Wazee hao wameomba kuwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya wazee hususani ugonjwa wa tezi dume.
Kuhusu watumishi wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Dkt. Kigwangala amesema Wizara itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili ili waweze kutekeleza majukumu yao vema. Katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Afya ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni la wazee wa kituo cha Wazee Kolandoto, bweni litakalobeba wazee 20. Pia amefungua jiko la gesi, amekabidhi bajaji pamoja na kiboksi cha huduma ya kwanza kwa wazee hao.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga