- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, amewasihi wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kuenzi na kudumisha Muungano uliosimikwa na waasisi wa taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Mhe. Macha ametoa wito huu leo, Aprili 26, 2025, wakati akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Shinyanga katika maadhimisho ya miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanyika katika mtaa wa Mabambasi, kata ya Ndembezi. Maadhimisho hayo yameambatana na shughuli za usafi wa mazingira na upandaji miti, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Muungano wa Tanzania ni wa kihistoria katika bara la Afrika. Nchi kadhaa zilijaribu kuungana lakini muungano wao haukudumu. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndio muungano wa kipekee uliojaa amani na mshikamano. Niwasihi wananchi waendelee kuuenzi Muungano huu kama ilivyokuwa dhamira ya waasisi wetu,” amesema Mhe. Macha.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amewasihi wakazi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,awamu ya pili linalotarajiwa kufanyika Mei 1-7, 2025. Kwa mkoa wa Shinyanga ambapo amesema zoezi hilo ni muhimu ili kuwawezesha wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia kupiga kura katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025 na kuwachagua viongozi bora wa kuliongoza taifa kwa kipindi kijacho.
Naye Mkuu wa Idara ya Maliasili na Mazingira Manispaa ya Shinyanga, Ndg. Ezra Manjerenga, ameeleza kuwa katika kuhakikisha miti inayopandwa inastawi vizuri na kuhifadhiwa, Halmashauri imekuja na kaulimbiu isemayo, “MTU NA MTI, MTI NA MTU”, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuimarisha utunzaji mazingira na kuhimiza ushiriki wa wananchi katika utunzaji wa mazingira yao.
Maadhimisho ya Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mwaka 2025 yanaongozwa na Kauli mbiu isemayo “Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu kwa Taifa: Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga