- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko amezindua Machinjio ya Kisasa ya ng’ombe na mbuzi yaliyopo katika kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga huku akitoa agizo kwa Wachinjaji katika mitaa mbalimbali Mjini Shinyanga kuhamia katika machinjio hayo mapya ambayo yanafuata taratibu zote za afya.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu Novemba 22,2021 na kuhudhuriwa na viongozi na wananchi wa Manispaa ya Shinyanga waliokuwa na kiu kubwa ya kuona machinjio hiyo inaanza kufanya kazi ili wapate fursa mbalimbali pamoja na kupata kitoweo kilichoandaliwa katika mazingira safi na salama.
“Tumezindua Machinjio haya kwa kuchinja ng’ombe wanne leo,hatukuwahi kufanya uchinjaji lakini baada ya kufanya zoezi hili tumebaini uwepo wa changamoto za kitaalamu hali inayosababisha leo zoezi litumie muda mrefu.Tutarekebisha changamoto zilizojitokeza na kesho Jumanne Novemba 23 tutaanza rasmi uchinjaji ambapo kazi itafanyika kwa kasi zaidi”,amesema Mboneko.
“Naomba tutumie machinjio haya kwani nyama inayotoka hapa itakuwa na ubora mkubwa iliyoandaliwa katika mazingira bora yanayozingatia kanuni na taratibu za afya. Machinjio zote zilizopo huko mtaani tunazifunga wiki hii ili wachinjaji wote wahamie hapa”,amesema Mboneko.
Mkuu huyo wa wilaya pia amesisitiza matumizi ya magari katika kusafirisha nyama badala ya kutumia matoroli na mifuko ili kuhakikisha nyama zinakuwa salama na bora kwa matumizi ya binadamu.
Aidha amewakaribisha wafanyabiashara wa ng’ombe na mbuzi ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga kutumia machinjio hiyo kuchinja mifugo na kusafirisha nyama badala ya kusafirisha wanyama wakiwa hai.
Mboneko amewahamasisha wakazi wa eneo la Ndembezi kuchangamkia fursa zinazopatikana katika machinjio hayo ikiwemo ajira zisizo za kitaalamu huku akiwasisitiza kuwa waadilifu na waaminifu kwa kufika kazini kwa wakati na kuepuka udokozi wa nyama katika machinjio hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura amesema mpaka sasa mradi huo wa Machinjio ya Kisasa umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 5.2 huku akieleza kuwa mradi huo ulichelewa kuanza kutokana na changamoto ya Mfumo wa Majitaka na Mfumo wa Ubaridi (Cold Room) na baada ya kuzitatua uchinjaji umeanza na wanategemea kuchinja kwa kasi zaidi kuanzia kesho Jumanne.
Mwenyekiti wa Wachinjaji mkoa wa Shinyanga, Masaka Charles amesema kutokana na kuzinduliwa kwa machinjio hiyo wachinjaji wote Mjini Shinyanga watahamia hapo ili kuendesha shughuli za uchinjaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga Mhe. Abubakar Mukadam amesema machinjio hiyo imeanza kufanya kazi baada ya serikali kutatua changamoto zilizokuwepo huku akitaka siasa kutoingizwa kwenye mradi huo.
Diwani wa kata ya Ndembezi Mhe. Victor Mmanywa ameshukuru kuzinduliwa kwa machinjio hiyo ambayo itawezesha wakazi wa kata ya Ndembezi kupata fursa mbalimbali.
Nao wakazi wa Ndembezi wameeleza kufurahishwa na kuanza kazi kwa machinjio hiyo wakisema matumaini yao ni kupata fursa za ajira.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga