- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Katika kuhakikisha ustawi, ulinzi na usalama wa watoto unaimarika katika Manispaa ya Shinyanga, shirika lisilo la kiserikali la Railway Children Africa limeendesha mafunzo maalum kwa wadau wa sekta ya ustawi wa jamii na ulinzi wa mtoto. Mafunzo haya yanalenga kuongeza uelewa wa namna ya kushughulikia tatizo la ukatili wa kijinsia pamoja na ongezeko la watoto wa mitaani.
Mafunzo hayo yamefanyika leo, Juni 19, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Lewis Kalinjuna, yakihusisha maafisa ustawi wa jamii, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wadau wa maendeleo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi uanzishwaji wa dawati la huduma za ustawi wa jamii katika vituo vya mabasi, mradi unaolenga kutoa huduma za kijamii katika vituo vya mabasi, ambapo watoto wanaoishi mitaani hukutanishwa kwa wingi.
Akizungumza katika mafunzo haya Meneja wa Mradi kutoka Railway Children Africa Bi. Irene Wampembe, amesema shirika hilo limejikita zaidi kutoa elimu na msaada kwa watoto wanaoishi mitaani, hususani katika maeneo ya vituo vya mabasi ambako hukusanyika watoto kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, huku akiongeza kuwa maeneo hayo yameonekana kuwa kiini cha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Awali mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Ndg. Revocatus Lutunda akifungua rasmi mafunzo hayo, amesema swala la ulizi na usalama wa mtoto ni la jamii nzima hivyo jamii inatakiwa kushirikiana ili kukomesha ongezeko la Watoto wa mtaani.
Naye, Afisa Ustawi dawati la ustawi wa jamii standi ya mabasi Manyoni, Bi. Penuela Samwel, ameeleza kuwa mpaka sasa, watoto 18 na watu wazima 20 wamepatiwa huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha tena na familia zao. Huku akiwahimiza wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto katika maadili mema.
Katika kuunga mkono juhudi za utekelezaji wa mradi huo, Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa tayari imefungua ofisi ndogo katika kituo kikuu cha mabasi cha Mkoa wa Shinyanga, kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma za kijamii na kusaidia shirika kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga