- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko amekabidhi Mikopo ya Ths. Mil 156.4 (Tsh. 156, 454,000/=) iliyotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa Vikundi 11 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kutoka kata mbalimbali ikiwa ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashari kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2021/2022.
Mbali na kukabidhi mkopo huo, Mboneko pia amekabidhi baadhi ya vifaa vya usafi kwa vikundi ambavyo vilipatiwa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kutoka Halmashauri.
Akizungumza wakati wa kukabidhi Mikopo hiyo, Mboneko amewataka wanakikundi hao kwenda kutumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili vikundi vingine vipatiwe mkopo huo.
“Fedha hizi tunazowapa zikafanye kazi kweli kweli ili muwa mfano, nendeni mkafanye kazi kwa ushirikiano na mshikamano. Na endapo mtapata changamoto toeni taarifa. Unapopata changamoto sema”,amesema Mboneko.
“Nanyi Maafisa Maendeleo ya jamii hakikisheni mnasimamia vikundi hivi na muwape elimu namna ya kuendeleza miradi yao”,amesema Mboneko.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Ramadhani Masumbuko amesema halmashauri hiyo itaendelea kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwani lengo ni kuwezesha wananchi wapige hatua kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Jomaary Satura, amesema Halmashauri imenunua eneo kwa ajili ya Wajasiriamali wa Kitangili ili kuwawezesha kufanya shughuli zao na kuhakikisha vikundi vyote vinanufaika na mikopo.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, John Tesha amesema kikundi cha NDEIMA wamekipatia mkopo wa Shilingi 80,454,000/= pamoja kukieleza kufanya shughuli zao ndani ya eneo hilo lililonunuliwa na Halmashauri kwa muda wa miaka mitatu.
Mbali na kikundi cha NDEIMA pia wametoa mikopo kwa vikundi vingine 10 vikiwemo vikundi vine vya watu wenye ulemavu hivyo kufanya idadi ya vikundi vilivyopewa mikopo kuwa 11 vyote vikipata mkopo wa jumla ya shilingi milioni 156.4.
“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha wanavikundi wote wanaokopeshwa na wale waliokwishakopeshwa wakumbuke kuwa mikopo hii wanayopatiwa lazima ikatekeleze miradi iliyoombwa na siyo vinginevyo. Kutotekeleza miradi waliyoombea mikopo au kubadilisha miradi iliyoombewa mikopo ni kinyume cha sheria na watachukuliwa hatua kali. Na vikundi ambavyo havitarejesha mikopo navyo vitachukuliwa hatua za kisheria”,amesema.
Mikopo hiyo imekabidhiwa Jumanne ya Septemba 27, 2022 katika kata ya Kitangili, eneo la ghala la kuhifadhia mazao lililonunuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ambalo ndani yake kuna mashine ya kukoboa nafaka, visima vya maji, banda la kufugia kuku, ofisi ndogo, wanyama na mabwawa ya kufugia samaki linalosimamiwa na Muunganiko wa vikundi vitatu vya Wanawake vya Ndembezi, Ibadakuli na Masekelo ambavyo kwa jina moja vinajulikana kama NDEIMA.
Tanesco S, Mwanza Road
Anwani ya Posta: P.O.Box 28 Shinyanga
Simu: +255-28-2763213
Simu ya Mkononi: 0759 023 788
Baruapepe: md@shinyangamc.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa@2018.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga